Idara
ya Uhamiaji katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imetoa siku tatu kwa
watumishi wake walioripoti Dodoma kuhamia katika nyumba zake zilizopo eneo la
Iyumbu, nje kidogo ya Manispaa ya Dodoma, badala ya kung’ang’ania kuishi
katikati ya mji.
Nyumba hizo 63 zenye
thamani ya Sh. bilioni 3.8 zimekabidhiwa jana kwa Idara hiyo na Shirika la
Nyumba (NHC).
Akizungumza katika
makabidhiano hayo, Kamishna wa Fedha wa Idara hiyo, Peter Chogero, kwa niaba ya
Kamshina Mkuu alisema serikali imeshanunua nyumba kwa ajili ya watumishi hao
hivyo hakuna sababu ya wao kuendelea kuishi katikati ya mji wa Dodoma.
“Uhamiaji imenunua
nyumba 63 eneo la Iyumbu ambazo zimejengwa na NHC, tutashangaa kuona watumishi
wengine waendelee kuishi mjini wakati nyumba zao zipo hapa Iyumbu,” alisema.
Alitoa siku tatu
kuanzia jana kila mtumishi aliyepangwa kuhamia kwenye nyumba hizo awe ameingia
kwa kuwa hakuna sababu ya kung’ang’ania kuishi nje ya nyumba hizo wakati
zimelipiwa na serikali.
Chongero alisema kabla
ya manunuzi ya nyumba hizo, Idara hiyo ilikuwa na nyumba 10 mjini Dodoma ambazo
hazikuweza kutosheleza watumishi wote, ikiwamo waliohamia kutoka Makao Makuu
Dar es Salaam.
Alibainisha waliamua
kuongeza idadi ya nyumba ili kila mtumishi wa Uhamiaji aishi kwenye nyumba ya
serikali na kwamba wanatarajia kuongeza nyingine 40.
Naye, Meneja Masoko wa
NHC, Itandula Gambalagi alisema ujenzi wa nyumba za Uhamiaji ulianza Desemba,
2016 katika eneo lenye ukubwa wa ekari 234 na ni moja ya sehemu ya mji
uliopangiliwa kitaalamu kwa kuzingatia sheria na kanuni za mipango miji.
Alisema nyumba
zilizokabidhiwa Uhamiaji ni sehemu ya nyumba 150 zilizojengwa katika mradi wa
Iyumbu na tayari nyumba zilizobaki zote zimepata wanunuzi.
Gambalagi alisema nyumba
hizo zina miundombinu yote inayotakiwa.
Kwa upande wake,
mthamini wa mali za serikali, Joseph Maliti aliagiza Uhamiaji kuingiza nyumba
hizo katika daftari la mali za serikali mara moja, ikiwa ni pamoja na thamani
kwa kila nyumba.
Post a Comment