Siku
35 baada ya Tundu Lissu kusema mwili wake bado una risasi moja baada ya
kutolewa nyingine 15, jana mbunge huyo wa Singida Mashariki (Chadema) alisema
kuwa madaktari wamemtoa kipande cha risasi kilichokuwa mwilini mwake.
Hata hivyo, mwanasheria
huyo mkuu wa Chadema, ambaye alishambuliwa kwa zaidi ya risasi 30 akiwa ndani
ya gari lililokuwa nje ya makazi yake mjini Dodoma Septemba 7 mwaka jana,
alisema chuma hicho ni tofauti na risasi aliyonayo mwilini, ambayo alielezwa na
madaktari wa Hospitali ya Nairobi, Kenya kuwa iko sehemu mbaya, lakini
isipotolewa haiwezi kumdhuru.
“Madaktari wamenitoa
kipande cha chuma katika sehemu ya makalio ambacho nilipokuwa Nairobi (Kenya)
madaktari walikiona lakini kilikuwa ndani ya nyama wakashindwa kukitoa,”
alisema Lissu
“Kipande hiki kilisogea
na wamekitoa. Ni tofauti na ile risasi ambayo iko mwilini mwangu.”
Akieleza kiundani
kuhusu hali yake, Lissu alisema anaendelea vizuri.
“Huu mkono wa kushoto
ambao ulikuwa na tatizo, wameunyoosha na kuufanyia mazoezi kweli kweli na huu
mguu wa kulia ambao ndio wenye tatizo, unaendelea vyema,” alisema.
“Huku ni mazoezi tu.
Kwa siku nafanya mazoezi kwa saa nne, Naingia saa 3:00 asubuhi hadi saa 4:00
asubuhi, narudi tena saa 5:00 asubuhi hadi saa 6:00 mchana. Mwisho naingia
mazoezini saa 8:00 mchana hadi saa 10:00 jioni. Hiyo ndiyo ratiba yangu kwa
siku.”
Alisema katika mazoezi
hayo anatumia magongo maalumu pamoja na kiti cha magurudumu.
“Mfano, huu mguu wa
kulia natakiwa kuukanyagia kwa kilo 20 hadi 25 katika mzani na mimi nina kama
kilo 90. Ninapoukanyagia ninaulizwa kama unauma, ikiwa sijasikia maumivu ina
maana sijafanya kitu, kwa hiyo ni kazi kwelikweli,” alisema.
Kuhusu muda ambao
anatakiwa kufanya mazoezi hayo mpaka atakaporejea katika hali yake ya kawaida,
Lissu alisema bado hajajua.
“Ah bwana we, hapa
madaktari wamegoma kunieleza hilo, lakini wameangalia katika maungio ya goti la
mguu wa kulia kuna mfupa haujaunga vizuri, ni lini utaunga hilo sijajua,”
alisema.
Mara baada ya
kushambuliwa kwa risasi na watu ambao hadi sasa hawajajulikana, Lissu
alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma kwa matibabu ya awali kabla ya
kuhamishiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya siku hiyo usiku.
Desemba 21 mwaka jana
wakati akihojiwa na kituo cha televisheni cha Azam, Lissu alisema madaktari wa
Nairobi walimueleza kuwa risasi iliyokuwa imesalia mwili haina madhara.
Alisema risasi saba
zilitolewa na madaktari hao, jambo lililomaanisha kuwa risasi nyingine nane,
zilitolewa na madaktari wa Tanzania, saa chache baada ya kushambuliwa
alipofikishwa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.
Post a Comment